IQNA

China yafunga duka la vitabu vya Kiislamu Beijing, mmiliki akamatwa

14:12 - October 11, 2017
Habari ID: 3471212
TEHRAN (IQNA)-Serikali ya China imefunga duka moja maarufu la vitabu vya Kiislamu na kumtia mbaroni mmiliki wa duka hilo kwa tuhuma za ugaidi.

Mfanyakazi mmoja wa Duka la Vitabu la Qingzhen katika eneo la Haidan mjini Beijing amethibitisha Jumanne hii kuwa duka hilo limefungwa na maafisa wa serikali.

MmiliKi wa duka hilo, Ma Yinglong, ambaye ni wa kabila la Dongxian katika jimbo lenye Waislamu wengi la Xinjiang, anashikiliwa na maafisa wa usalama kwa tuhuma za ugaidi.

Taarifa zinasema Ma aliwahi kushikiliwa kwa muda wa mwaka moja kwa tuhuma za kujihusisha na biashara zilizo kinyume cha sheria na kwamba alikuwa ameachiliwa kwa muda.

Duka la vitabu la Qingzhen huchapisha na kuuza vitabu kuhusu Uislamu na maudhui husika. Vitabu hivyo pia huuzwa katika tovuti ya IslamBook.net na huwa na maudhui anuai kuanzia filosofia ya Kiislamu hadi maisha ya Waislamu chini China. Tovuti hiyo ya lugha ya Kichina imefungwa ndani ya China kwenyewe na ni watu walio nje ya China wanaoweza kuisoma.

Mtetezi wa haki za binadamu nchini China, Liu Zinglian ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu katika jimbo la Hainan anasema wakuu wa China sasa wanauhusisha Uislamu na ugaidi ili kuwazuia wanaharakati kama vile mwanazuoni wa Kiislamu wa kabila ya Uyghur, Sheikh Ilham Tohti kuzgunzma dhidi ya ukandamizaji wa serikali.

Hayo yanajiri siku kadhaa baada ya polisi katika mkoa wa Xinjiang kaskazini magharibi mwa China wameamuru familia za Waislamu kukabidhi madhihirisho ya kidini hasa nakala za Qur'ani na misala.

Hii si mara ya kwanza kwa wakuu wa mkoa wa Xinjiang nchini China kuwakandamiza Waislamu. Mwaka jana watawala wa eneo hilo waliwaamuru wanafunzi, wafanya kazi wa umma na hata wakaazi wa kawaida kutofunga saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Aidha Waislamu wa eneo hilo walipigwa marufuku kuwapa watoto wao baadhi ya majina ya Kiislamu

Chama tawala cha Kikomunisti cha China kwa miaka kadhaa sasa kimekuwa kikiwakandamiza Waislamu katika eneo la Xinjiang.

3464144

captcha