IQNA

Katibu Mkuu wa OPEC: Haiwezekani kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la dunia

9:18 - May 04, 2019
Habari ID: 3471940
TEHRAN (IQNA)- Hatua ya serikali ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vya mafuta baada ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA imekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanunuzi wa mafuta ghafi ya petroli ya Iran katika soko la kimataifa na pia kutoka kwa wakuu wa Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC).

Katibu Mkuu wa OPEC, Mohammed Sanusi Barkindo, akizungumza pembizoni mwa Maonyesho ya 24 ya Mafuta, Gesi na Petrokemikali ya Iran yanayofanyika Tehran alisema: "Changamoto kuhusu mafuta ya Iran si ya nchi moja tu bali pia OPEC nayo inaathirika. Kile kinachofanyika Iran, Venezuela na Libya kitakuwa na taathira hasi katika soko na sekta ya mafuta. Ameongeza kuwa, "Tumekuwa na changamoto nyingi katika kipindi cha miaka 60 iliyopita ndani ya OPEC, lakini changamoto hizo tukazipatia ufumbuzi kwa ushirikiano."

Utawala wa Rais Trump wa Marekani umedai kuwa, kwa kuiwekea Iran vikwazo vya kuuza mafuta katika soko la dunia, vikwazo ambavyo vilianza Novemba 2018, hatimaye uuzaji mafuta ya Iran utafika sifuri kuanzia Mei 2 2019. Madai hayo ya Trump si  tu kuwa yamekosolewa na wataalamu wa soko la mafuta bali hata pia wakuu wa OPEC. Akijibu swali kuhusu iwapo  kuna uwezekano wa kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la kimataifa, Katibu Mkuu wa OPEC amesema: "Hakuna haja ya kujikariri. Kimsingi ni jambo lisilowezekana kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la dunia.

Aprili 22, Marekani iliziagiza nchi nane ambazo ilikuwa imeziruhusu kuendelea kununua mafuta ya Iran licha ya vikwazo vyake ziache kuagiza bidhaa hiyo kuanzia Mei Mosi, vinginevyo itaziwekea vikwazo.

Hatua hiyo ya Trump imechukuliwa katika fremu ya 'mashinikizo ya juu kabisa' ili kuishinikiza Iran kiuchumi kwa kukata vyanzo vyake vyote vya fedha ambavyo vinatokana na uuzaji mafuta katika soko la kimataifa. Lengo la Marekani ni kuishurutisha Iran isalimu amri na ikubali masharti 12 ambayo Washington imeiwekea.

Umoja wa Ulaya waikosoa Marekani

Uhasama huo wa Marekani umekosolewa vikali kimataifa, katika taasisi mbali mbali na pia katika vyombo vya habari. Aghalabu ya weledi wa masuala ya mafuta na pia wataalamu katika taasisi za  nchi za Magharibi wanaamini kuwa, uamuzi wa Marekani wa kubatilisha idhini kwa wanunuzi wa mafuta ya Iran ni hatua ambayo itaathiri vibaya sana soko la mafuta ghafi ya petroli duniani katika kipindi cha miezi ijayo. Benki ya Barclays imetabiri kuwa, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu haziwezi kujaza pengo la mafuta ya Iran katika soko la kimataifa kama zinavyodai. Aidha benki hiyo imesema maamuzi ya Marekani yanaibua hatari ya kuwepo mapigano Asia Magharibi hasa uwezekano wa kufungwa Lango Bahari la Hormoz. Hali kadhalika radiamali ya wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Iran kama vile China na India nayo itakuwa na umuhimu mkubwa.

Hali kadhalika nchi za Ulaya zina wasi wasi mkubwa kutokana na taathira hasi za vikwazo vya mafuta ya Iran katika mapatano ya nyuklia ya Iran. Miguel Arias Canete, Kamishna wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya nishati, siku ya Alhamisi akizungumza katika kikao cha waandishi habari akiwa ameandamana na Rick Perry Waziri wa Nishati wa Marekani alikosoa vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran na kusema: "Tangazo la Marekani kutorefusha muda wa kununua mafuta ya Iran ni jambo ambalo litadhoofisha utekelezwaji wa mapatano ya JCPOA. Mapatano ya JCPOA ni moja ya misingi muhimu ya kuzuia uenezwaji silaha za nyuklia na ni mapatano ambayo yameidhinishwa na Baraza la Usalama na yana umuhimu mkubwa kwa eneo na dunia nzima."

Nchi za Ulaya zinafahamu vyema kuwa iwapo mapatano ya JCPOA hayatakidhi matakwa na matarajio ya Iran baada ya kuanza tena kutekelezwa vikwazo vya Marekani basi haiwezi kutarajiwa kuwa Iran itaendelea kutekeleza mapatano hayo ya JCPOA.

Kuhusiana na nukta hii, Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa subira ya Iran inakaribia kufika ukingoni.

3808442

captcha