IQNA

Nabii Isa Masiih AS, Mja wa Mwenyezi Mungu

16:27 - December 25, 2018
Habari ID: 3471786
TEHRAN (IQNA) Leo Disemba 25 inasadifiana na siku aliyozaliwa Nabii Isa Masiih- Amani Iwe Juu Yake (AS) kwa mujibu wa imani ya Wakristo waliowengi.

Mtume huyo mwema alikuwa mtoa bishara njema na mlinganiaji wa kweli na upendo na itikadi na Mungu Mmoja. Isa Masiih alizungumza kwa amri ya Mwenyezi Mungu akiwa katika susu na kuwaambia watu waliokuwa katika mghafala wa zama hizo kama inavyotwambia aya ya 30 hadi 33 za Suratu Maryam kwamba: Na akasema: Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na kunifanya Nabi. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo na ameniusia Swala na Zaka maadamu ni hai. Na kumtendea wema mama yangu. Wala hakunifanya jeuri, muovu. Na amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa."

Zama za kuzaliwa

Nabii Isa alizaliwa katika zama ambazo makundi mbalimbali ya Kiyahudi yalikuwa yamezama katika hitilafu na migawanyiko mikubwa. Makundi mawili makuu ya Wasadukayo (Sadducees) na Mafarisayo (Pharisees) yalikuwa yakidhibiti na kutawala itikadi za watu wa zama hizo. Wasadukayo (Sadducees) lilikuwa kundi la mabwanyenye na aghlabu yao walikuwa makuhani na wanazuoni wa kidini ambao walikuwa wakishirikiana na utawala wa kifalme wa Roma kwa ajili ya kulinda mafundisho na ada za kidini na hawakukabiliana kwa njia yoyote ile ya utamaduni wa Kigiriki. Hii ni kwa sababu walikuwa wakiamini kwamba, Mwenyezi Mungu pia ameeneza maadili ya Kitabu Kitakatifu kati ya wasio Wayahudi. Mkabala wake, Mafarisayo (Pharisees) lilikuwa kundi lisilo la makuhani lakini lenye ushawishi mkubwa zaidi kuliko Wasadukayo (Sadducees). Kundi hili liliamini kuwa, kaumu ya Mayahudi inapaswa kuwa kaumu tofauti na iliyojitenga na kaumu nyinginezo na haipasi kufuata kaumu hizo au kuchanganyika nazo. Kundi la Mafarisayo (Pharisees) lilikuwepo katika maeneo yote ya Palestina na lilidhibiti masinagogi na maabadi zote za nje ya Baitul Muqaddas (Jerusalem) ambako Wayahudi walikuwa wakikusanyika kwa ajili ya ibada au kusoma.

Mayahudi wenye misimamo mikali

Mbali na makundi hayo mawili makuu, kulikuwepo makundi mengine kama Samaritans (Wasamaria) na kundi la Wayahudi wenye misimamo mikali lililokuwa maarufu kama Zealots. Wasamaritani katika mtazamo wa makundi mengine, walitambuliwa kuwa makafiri, na Zealots lilikuwa kundi la Wayahudi wenye misimamo ya kuchupa mipaka la kisiasa lililokuwa likiwachochea Wayahudi kuwafukuza kwa mabavu na kwa njia za mauaji ya kigaidi Warumi na utawala wao katika ardhi ya Palestina. Kundi hili halikushambulia Warumi pekee, bali hata Wayahudi wenzao ambao kwa madai yao, hawakuwa na ghera ya kutosha ya udini na utaifa.

Nabii Isa Masih alizaliwa katika mazingira kama haya. Wakuu wa kaumu ya Mayahudi katika kila kundi walijua vyema sifa na alama zake kutokana na utabiri wa hapo kabla na habari walizosoma na kukusanya katika vitabu vya kale. Hata hivyo walipuuza utabiri na alama hizo tangu hapo mwanzoni na kukabiliana na Nabii huyo mkubwa wa Mwenyezi Mungu. Hatua ya kwanza kabisa ya Mayahudi hao ilikuwa kumtuhumu mama yake Masih, Bibi Maryam AS kuwa ni fasiki ili wapate kumrujumu kadamnasi. Hata hivyo njama hiyo ilifeli, na Isa na mama yake, Bibi Maryam wakaokoka kifo na vitimbi vya Mayahudi baada ya Masih kuzungumza akiwa kwenye susu na kusema: "Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na akanijaalia kuwa Nabi.."

Jitihada kubwa za kuongoza watu katika haki

Nabii Isa AS alibaathiwa na kuamrishwa kutangaza ujumbe wa Mwenyezi Mungu baina ya Banii Israel akiwa na umri wa karibu miaka 30. Alifanya jitihada kubwa za kuwaongoza katika kweli na haki na kuwaondoa katika upotovu. Aliwabainishia halali na haramu na kuwahalalishia mengi waliyokuwa wamekatazwa. Kwa mujibu wa Injili ya Mathayo 4/17 ni kwamba Isa alianza kuhubiri kwa kusema: “Tubuni, kwa sababu Ufalme wa mbinguni umekaribia.”

Mbali na kuwaongoza watu katika njia ya haki, Nabi Isa alikuwa akitibu wagonjwa. Alikuwa akitibu vipovu na barasi au mbalanga na kufufua wafu kwa uwezo wake Mola Muumba. Vilevile alikuwa akitengeneza ndege kutoka kwenye udongo. Daima alikuwa msaidizi wa watu waliokuwa wakidhulumiwa na kukandamizwa na aliwakirimu na kuwafanyia ihsani sana watoto na wanawake. Wakati huo huo alipinga vikali sheria kali za baadhi ya Mafarisayo (Pharisees) na misimamo ya kuchupa mipaka ya Zealots.

Mashaka na tabu

Nabii Isa AS alipata mashaka na tabu kubwa katika kuwaongoza Wayahudi na kuwaelekeza katika njia sahihi. Katika mashaka hayo alielewa kwamba, Wayahudi wanashikilia maasi na hawakuwa tayari kuachana na dhambi na njia potovu. Alisimama katika kaumu yake na kusema: "Nani kati yenu atakayenisaidia katika njia ya Mwenyezi Mungu?" Watu wachache kati ya Mayahudi walijitokeza na kuitikiwa wito wake. Kundi hilo lilikuwa na watu wasafi ambao Mwenyezi Mungu SW anawataja katika Qur'ani tukufu kwa jina la "Hawariyyun". Kundi hili la Hawariyyun lilitangaza utayarifu wao wa kumsaidia Nabi Isa Masih katika njia ya Mwenyezi Mungu kama inavyosimilia Qur'ani tukufu katika aya ya 52 hadi 53 za Suratu Aal Imran zinazosema: "Isa alipohisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemwamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba, sisi hakika ni Waislamu. Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia."

Isa na wanafunzi wake hao walielekea katika maeneo ya kaskazini mwa Palestina na kuwafundisha watu dini halisi ya Mwenyezi Mungu. Maarifa ya dini yaliyofundishwa na Nabi Isa yaliwashangaza wengi na kuwakasirisha wanasiasa waliokuwa wakitawala jamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Nabii huyo mwema wa Mwenyezi Mungu alipinga vikali tabia ya watawala na makuhani wa dini ya Kiyahudi ya kuzama katika anasa na dunia. Hakuvumilia ufuska na ufisadi wa aina yoyote na kwa msingi huo makundi yote ya Wayahudi yalianza kumkadhibisha na kumpiga vita. Makundi hayo yalitayarisha uwanja na mazingira ya kumuua mjumbe huyo mwema wa Allah SW. Ili kufikia lengo hilo chafu, Mayahudi hao walimchochea Kaizari wa Roma na kumwambia: "Kama hali hii itaendelea, ufalme wako pia utatoweka, hivyo ili kulinda utawala na ufalme wako huna budi kumuua Masia!"

Hakusulubiwa

Isa Masih AS aling'amua njama yao na akajificha katika shamba moja akiwa pamoja na Hawariyyun na wanafunzi wake. Hata hivyo mtu mmoja kati ya wanafunzi wake aliyejulikana kwa jina la Yuda aliwaonesha maadui mahali lipokuwa amejificha. Maafisa wa utawala walivamia eneo hilo nyakati za usiku na kulizingira. Wanafunzi wa Isa Masih walipohisi hatari walimkimbia na kumuacha peke yake, lakini Mwenyezi Mungu SW kamwe hakumuacha peke yake Mtume wake mwema katika kipindi hicho hatari. Mwenyezi Mungu SW alimlinda Mtume wake na kumdhihirisha Yuda aliyekuwa akifanya ujasusi dhidi ya Nabii huyo, katika sura ya Isa, na maadui wakamkamata yeye wakidhani kuwa ni Masih. Yuda alichanganyikiwa kutokana na hofu na machungu mengi na hatimaye akashindwa kuzungumza na kujiarifisha. Hata wakati alipoweza kufungua mdomo na kuzungumza, hakuna mtu aliyekuwa tayari kukubali maneno yake. Yuda alipandishwa msalabani na kusulubiwa. Watu walioshuhudia tukio hilo wote walidhani kuwa Isa Masih AS ameuawa, lakini kama inavyosisitiza Qur'ani tukufu, Nabii huyo mwema wa Mwenyezi Mungu hakusulubiwa wala kuuawa. Aya za 157 na 158 za Suratu Nisaa zinasema: Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masih Isa, mwana wa Maryam, Mtume wa Mwenyezi Mungu -, nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima"

Baada ya Nabii Isa Masih kuinuliwa na kupelekwa mbinguni, wanafunzi wake walidumisha njia yake ya kuwaongoza watu. Kati ya wanafunzi hao, Peter ambaye alikuwa wa kwanza kumwamini Masih AS alipewa jukumu la kuwaongoza Mayahudi na kusimamia wanafunzi wengine. Aliwatuma Hawariyyun katika maeneo mbalimbali ya dunia kuongoza kaumu mbalimbali za Bani Israel kwa mujibu wa mafundisho ya Isa AS.

Upole na unyenyekevu

Sambamba na kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnsaba wa kuadhimisha tukio la kuzaliwa Nabii Isa Masih AS, tunakamilisha kipindi chetu hiki kwa kusimulia kisa cha maisha ya unyenyekevu na upole wa Mtume huyo adhimu wa Mwenyezi Mungu.

Siku moja Isa Masih alikwenda kwa wanafunzi wake na kuwaambia: Nina haja na kama mnaahidi kunikidhia nitawaambia. Hawariyyun walisema: "Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu! Tuko tayari kutii na kutekeleza amri yako." Isa AS aliinuka na kisha akaelekea upande wao na kuanza kuosha miguu ya kila mmoja wao. Hawariyyun waliona haya na kujihisi vibaya, lakini walisalimu amri na kumuacha Issa Masih akiosha miguu yao, kwa kuwa walikuwa tayari wameahidi kutii na kukidhi haja yake. Baada ya kukamilisha kuosha miguu yao, Hawariyyun walisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wewe ni mwalimu wetu na unastahiki zaidi tukuoshe miguu badala ya wewe kuosha miguu yetu." Mtukufu Isa Masih alisema: "Nimefanya hivi ili kuonesha unyenyekevu na kuwafunza jinsi ya kunyenyekea na kufanya tawadhu'i, na baada yangu mtakaposhika usukani wa kufunza na kuwaongoza watu, mutangulize mbele njia hii ya unyenyekevu na kuhudumia viumbe wa Mwenyezi Mungu. Kimsingi hekima inaota katika unyenyekevu na upole na si katika kiburi na majivuno, sawa kabisa na jinsi mimea inavyoota na kustawi katika ardhi nyororo na laini na si katika ardhi ngumu na miamba." 

 

captcha