IQNA

Inna Lillah wa Inna Ilayhi Rajioun

Waislamu wasiopungua 62 wauawa katika hujuma za kigaidi msikitini Afghanistan

22:14 - October 18, 2019
Habari ID: 3472176
TEHRAN (IQNA) - Waislamu wasiopungua 62 wameuawa na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa katika hujuma kadhaa za kigaidi zilizotokea leo ndani ya msikiti wakati wa Sala ya Ijumaa katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa Afghanistan.

Attaullah Khogyani, msemaji wa gavana wa Nangarhar amesema, watu wasiopungua 62 wameuawa katika miripuko iliyotokea wakati wa Sala ya Ijumaa ndani ya msikiti ulioko kwenye wilaya ya Haska Mena mkoani humo.

Sohrab Qaderi, mjumbe wa baraza la mkoa wa Nangarhar amevieleza vyombo vya habari kuwa, watu zaidi ya 100 wamejeruhiwa pia katika tukio hilo na kuna uwezekano idadi ya vifo ikaongezeka wakati timu ya uokoaji ikiwa inaendelea kutoa viwiliwili vilivyofunikwa na vifusi.

Shambulio hilo la leo limetokea siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kueleza kwamba machafuko nchini Afghanistan yamefikia kiwango ambacho "hakiwezi kukubalika."

Tangu Julai Mosi hadi Septemba 30 mwaka huu, watu 1,174 wameuawa na wengine 3,139 wamejeruhiwa, likiwa ni ongezeko la asilimia 42 kulinganisha na kipindi kama hicho katika mwaka uliopita, ambapo zaidi ya asilimia 40 ya walioathirika ni wanawake na watoto wadogo.

Wakati huohuo, msemaji wa kundi la Taliban Dhabihullah Mujahid, amelaani shambulio hilo la leo la kigaidi na kutangaza kuwa kundi hilo halijahusika kwa namna yoyote ile katika mashambulio hayo.

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, msemaji huyo wa Taliban amelibebesha dhima ya hujuma hiyo kundi la kigaidi na ukufurishaji la ISIS au Daesh.

Magaidi hao wakufurishaji la wa kundi la Kiwahhabi la ISIS wanaendesha harakati zake katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Nangarhar likiwemo la Achin.

Wakati huo huo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali hujuma hiyo dhidi ya Waislamu msikitini nchini Afghanistan. Sayyed Abbas Mousavi amesema kuwalenga Waislamu wakati wa Sala ya Ijumaa ni ishara kuwa magaidi wanalenga kuibua mifarakano baina ya Waislamu na kuvuruga uthabiti katika nchi hiyo ya Waislamu.

3469688

captcha