IQNA

Rais wa Iran katika mazungumzo ya simu na Rais wa Ufaransa

Muswada uliopendekezwa na Marekani katika Baraza la Usalama unakiuka JCPOA

10:51 - August 13, 2020
Habari ID: 3473063
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa ufaransa akisema kuwa Marekani daima imekuwa ikifanya jitihada za kuua mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa: Ulaya haipasi kukubali kuburutwa na Marekani na kutumbukia katika mtego wake.

Rais Hassan Rouhani amesema katika mazungumzo hayo yaliyofanya alasiri ya jana kwamba kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa tarehe 18 Oktoba. Amesisitiza kuwa: Muswada uliopendekezwa na Marekani katika Baraza la Usalama la UN unakiuka azimio nambari 2231, ambalo liliidhinisha mapatano ya JCPOA, na hivyo nchi zote hususan wanachama wa kundi la 4+1, zinapaswa kuupinga vikali.

Rais Rouhani ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kwamba zaidi ya miaka miwili iliyopita Marekani ilijiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, nchi hiyo haina tena haki ya kutumia vipengee vya makubaliano hayo. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua zinazokiuka sheria na zisizo za kibinadamu za Marekani za kuliwekea vikwazo taifa la Iran katika kipindi hiki kigumu cha maambukizi ya virusi vya corona na amesisitiza udharura wa Ulaya kuhuisha uhusiano wa kiuchumi na Iran na ushirikiano wa pande mbili katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Rais Rouhani pia ameashiria hali ya Lebanon baada ya mlipuko mkubwa uliotokea wiki iliyopita katika bandari ya Beirut na kusema: Lebanon inahtajia umoja na mshikamano baina ya makundi yote ya kisiasa, na pande zote zinapaswa kuimarisha umoja huo.

Kwa upande wake Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesisitiza umuhimu wa kulindwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: Mtazamo wa Ufaransa unatofautiana kikamilifu na ule wa Marekani katika suala la kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, na kwamba Paris imeieleza waziwazi Washington msimamo huo.

Macron amesema Ufaransa inafanya jitihada za kuanzisha mfumo wa kifedha baina ya Ulaya na Iran. 

Macron ameashiria safari yake ya siku kadhaa zilizopita nchini Lebanon na ameiomba Iran isaidia juhudi za kutatua mgogoro wa kisiasa nchini humo. Vilevile ameialika Tehran kushiriki katika kundi la kimataifa la kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Lebanon. 

3916319

captcha