IQNA

Ujumbe wa rais wa Iran kwa mnasaba wa Idul Adha

19:43 - July 21, 2021
Habari ID: 3474116
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu maalumu kwa viongozi wa nchi za Kiislamu kuwatakia kheri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha Sikukuu ya Mfunguo Tatu ya Idul-Adhha.

Katika salamu zake hizo, Rais Rouhani amewapa mkono wa Idi viongozi wa nchi za Kiislamu na kueleza kwamba, Sikukuu hii ni msimu wa kuyachinja mapenzi ya kidunia, kuuvua moyo na matashi kwa ajili ya Mola Mpendwa halisi wa mja na kudhihirika imani na utiifu halisi mbele ya Muabudiwa.

Rais Rouhani amesema, ana matumaini kuwa, kwa baraka za Sikukuu hii azizi na kwa kujivua pingu za hawaa na matamanio ya nafsi, kujitolea kwa hali na mali kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuwasaidia ndugu zao Waislamu na wanadamu wenzao, Waislamu wote wataweza kujikurubisha kwa Allah na kupata rehma zake Mola Aliyetukuka zisizo na mpaka.

Halikadhalika katika ujumbe wake huo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaombea uzima na mafanikio viongozi; na saada na izza wananchi wa mataifa ya Kiislamu.

Baadhi ya nchi ikiwemo Saudi Arabia, Palestina, Syria na Afghanistan zilisherehekea Sikukuu ya Mfunguo Tatu hapo jana, na katika baadhi ya nchi ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Idul-Adhha inaadhimishwa leo.

Idul-Adhha, yaani Sikukuu ya Kuchinja au Idul-Hajj ni miongoni mwa Sikukuu kubwa za Waislamu.

Katika siku hii tukufu, Mahujaji waliokwenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu huchinja kwa amri ya Mola na kwa ajili ya kupata radhi zake; na kwa kufanya hivyo, huendeleza na kuenzi kumbukumbu ya Mtume mteule wa Allah, Nabii Ibrahim (AS).

/3985503

captcha