IQNA

Hizbullah yalaani Israel kwa kuishambulia Syria na kukiuka anga ya Lebanon

22:28 - July 23, 2021
Habari ID: 3474121
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema, shambulio la karibuni la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria ni uchokozi na uvamizi wa waziwazi dhidi ya ardhi ya nchi hiyo na ardhi ya Lebanon.

Katika taarifa iliyotoa leo , Hizbullah imetangaza kuwa, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zimekiuka kwa mara nyingine tena mamlaka ya kujitawala ya Lebanon na kuishambulia Syria kwa kutumia anga ya nchi hiyo.

Katika taarifa yake hiyo, Hizbullah imelikosoa na kulilaumu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba, hatua vamizi na za kichokozi za utawala haramu wa Israel zinafanywa chini ya kivuli cha kimya cha jumuiya za kimataifa na wale wanaodai kuwa watetezi wa kulindwa na kuheshimiwa uhuru na mamlaka ya kujitawala ya mataifa.

Usiku wa kuamkia Alkhamisi ya jana, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia eneo la al Qasir, kwenye viunga vya magharibi ya mkoa wa Homs nchini Syria. Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo lilifanikiwa kuyateketeza katika anga ya mkoa huo wa Homs makombora kadhaa ya Israel kabla hayajapiga sehemu zilizokuwa zimelengwa.

Jumatatu iliyopita pia, utawala haramu wa Kizayuni ulifanya mashambulio ya anga dhidi ya mji wa As-Safirah ulioko kwenye kiunga cha kusini mashariki ya mkoa wa Aleppo.

Kufuatia mashambulio hayo , Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ililitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilaani uchokozi huo wa utawala wa Kizayuni na kuchukua hatua za kuzuia usirudiwe tena.

Ndege za kivita za utawala haramu wa Israel zimekuwa zikiitumia kinyume cha sheria mara kwa mara anga ya Lebanon au kupitia miinuko ya Golan ili kushambulia maeneo kadhaa ya masharki na kaskazini magharibi ya Syria.

3985807

captcha