IQNA

Ugaidi Afghanistan

Magaidi waua watu wasiopungua 32 katika hujuma Kabul, Afghanistan

20:45 - September 30, 2022
Habari ID: 3475857
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua 32 wameuawa katika shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu uliotokea mapema leo katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Katika miezi na wiki zilizopita Afghanistan imeshuhudia miripuko na mashambulizi ya kigaidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Kabul yaliyolenga misikiti ya Mazar-e-Sharif na Kunduz ambayo yamesababisha mamia ya watu kuuawa na kujeruhiwa. Kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) limekiri kuhusika na mashambulio mengi miongoni mwa hayo.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Al Jazeera, duru za Afghanistan zimetangaza kuwa, watu wengine 35 wamejeruhiwa kutokana na shambulio hilo la kigaidi la mripuko wa bomu uliotokea katika kituo kimoja cha mafunzo ya elimu magharibi mwa Kabul.
Ripoti hiyo ya Aljazeera imeongeza kuwa, baada ya mripuko huo, milio ya risasi ilisikika pia katika kituo hicho cha mafunzo.

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa, na hadi sasa hakuna mtu au kikundi kilichodai kuhusika na shambulio hilo.

Ijumaa iliyopita pia, watu wanne waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa katika shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu uliotokea karibu na lango la kuingilia msikiti wa eneo la Wazir Akbar Khan mjini Kabul. 
Kutokea miripuko ya kigaidi katika mikoa tofauti ya Afghanistan kunaonyesha kuwa, kinyume na madai ya serikali ya mpito ya Taliban, serikali hiyo haijaweza kudhamini usalama unaohitajika katika mji wa Kabul na miji mingine ya nchi hiyo.
3480674
captcha