IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran haijawahi kusalimu amri mbele ya nchi za Magharibi

19:49 - June 05, 2014
Habari ID: 1414443
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kusalimu amri mbele ya nchi za Magharibi na kwamba imeweza kustawi na kuendelea siku hadi siku.

Ameyasema hayo Jumanne mjini Tehran katika hafla ya kukumbuka kurejea kwa mola wake Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Wapenzi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) kutoka kila kona ya Iran walishiriki katika kumbukumbu za mwaka wa ishirini na tano wa kufariki dunia muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, zilizofanyika katika eneo alipozikwa mwanachuoni huyo mkubwa, na kuonyesha taswira isiyo na kifani ya hamasa, kusimama kidete, heshima na mapenzi yao kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na wakati huo huo kutangaza kwa mara nyingine tena utiifu wao kwa mwanachuoni huyo aliyetangulia mbele ya Haki.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alihudhuria hadhara hiyo kubwa iliyojaa nuru na kuhutubia hadhirina. Katika hotuba yake, amezungumzia asili na sababu ya kuongezeka kila leo hamu na mapenzi ya mataifa ya walimwengu ya kuusoma na kuzidi kuuelewa mfumo wenye nguvu kubwa na unaozidi kuimarika wa Jamhuri ya Kiislamu ambao umeiundwa juu ya msingi wa sheria za Kiislamu na demokrasia iliyotokana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Amesema sheria za Kiislamu na demokrasia ni vitu viwili vikuu vilivyomo kwenye chuo na aidiolojia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh). Vile vile amesisitiza kuwa, wananchi na viongozi wa Iran wameshikamana vilivyo na nakala hiyo mpya ya kisiasa - kijamii na kuongeza kuwa: Usumbufu na njama za kila namna zinazofanywa na Marekani na kupungua kasi ymoyo wa kuelekea kwenye mwamko wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) ni changamoto mbili kuu ambazo iwapo taifa la Iran litazitambua na kuzishinda, litaweza kuendeleza vizuri njia iliyojaa fakhari na ufanisi ya Imam (quddisa sirruh).
Katika sehemu ya kwanza ya hotuba yake mbele ya hadhara hiyo adhimu ya kitaifa, Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuzidi kuvutiwa walimwengu na hasa wa mataifa ya Waislamu na Imam Khomeini na Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni uhakika muhimu sana na kuongeza kuwa: Hivi sasa na baada ya kupita miaka 25 tangu afariki dunia Imam Khomeini (quddisa sirruh) matabaka mbali mbali ya watu hasa vijana na watu muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu wamezidi kuwa na hamu na shauku ya kuitambua zaidi aidiolojia ya demokrasia ya kidini, nadharia ya Fakihi Mtawala (Wilayatul Faqih) na masuala mengine yanayohusiana na Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameyataja mashambulizi yasiyosita na makubwa mno wa kisiasa na kipropaganda ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni moja ya sababu zilizoongeza hamu ya mataifa ya walimwengu kutaka kuyajua zaidi Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Fikra za walio wengi katika ulimwengu wa Kiislamu; hivi sasa na kuliko wakati mwingine wowote, zimekuwa na hamu kubwa zaidi ya kuujua wasifu na uhalisia wa mfumo wa kiutawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao unashambuliwa kwa mashambulizi makubwa kiasi chote hiki kutoka kila kona ya dunia na zina hamu na kuelewa siri ya taifa la Iran ya kuweza kusimama kidete na kupata mafanikio makubwa katika misimamo yake licha ya kukumbwa na dhoruba zote hizo za mashambulizi ya kila upande ya maadui.
Aidha ameutaja uwezo, nguvu na maendeleo yanayoongezeka kila leo ya taifa la Iran kuwa ni sababu nyingine inayoyafanya mataifa ya dunia yawe na shauku ya kuijua zaidi Jamhuri ya Kiislamu na mfumo wa demokrasia ya kidini unaotawala nchini Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mwamko wa Kiislamu na hisia za kupinga uistikbari na ubeberu kuwa ni moja ya matunda ya shauku na hamu ya mataifa hasa ya Kiislamu ya kuyatambua zaidi Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba: Kambi ya kibeberu, inaendelea kufanya makosa ya kiistrajitia kwa kudhani kuwa imeweza kung'oa mizizi ya mwamko wa Kiislamu kwani mtu anapoangalia kwa kina na kuelewa mambo yaliyopelekea kutokea mwamko wa Kiislamu atatambua vyema kuwa mwako huo si kitu kinachoweza kuondoka, na kwamba mwamko huo utachomoza tena na tena na kupanuka kwa nguvu za hali ya juu zaidi.
Amesema, kizazi cha vijana katika ulimwengu wa Kiislamu kinatafuta majibu ya maswali muhimu ya kihistoria kwamba kwa nini na kivipi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kusimama imara katika kipindi chote hiki cha miaka 35 licha ya kushambuliwa kutoka kila upande kiuadui, kijeshi, kisiasa na kipropaganda pamoja na kuwekewa mashinikizo na vikwazo vikubwa mno na Marekani ambavyo havijawahi kushuhudiwa mfano wake na wakati huo huo taifa la Iran kila leo likawa linazidi kupiga hatua za kimaendeleo na kuwa imara tena bila ya kuwa taifa la kihafidhina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kutoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazoifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na mvuto wa aina yake akisema: Mataifa ya dunia na kizazi cha vijana na tabaka la watu wenye ushawishi katika ulimwengu wa Kiislamu wanayaona maendeleo mbali mbali ya taifa la Iran katika nyuga za anga na anga za mbali, wanaona namna Iran ilivyo katika orodha ya nchi kumi za dunia zilizo na maendeleo makubwa sana ya kielimu, wanaona jinsi kasi ya maendeleo ya kielimu ilivyo mara 13 zaidi nchini Iran ikilinganishwa na wastani wa kasi hiyo duniani na wanatambua kuwa taifa la Iran ni nambari moja katika siasa za eneo la Mashariki ya Kati na limesimama imara katika kupambana na utawala ghasibu wa Kizayuni na kuyahami na kuyatetea mataifa yanayodhulumiwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mambo hayo humfanya kila mtu awe na shauku na hamu ya kutaka kuijua zaidi na zaidi Jamhuri ya Kiislamu.
Vile vile amekutaja kufanyika uchaguzi wa 32 katika kipindi cha miaka 35 iliyopita tena kwa kujitokeza kwa wingi wa kupigiwa mfano wananchi wa Iran katika uchaguzi huo, na kujitokeza kwa hamasa kubwa na kwa wingi mno wananchi wa Iran katika maandamano ya Bahman 22 ( Februari 11, zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu) na katika maandamano ya Siku ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani) kuwa ni uhakika mwingine unaozifanya fikra za walimwengu zivutiwe na Iran.
Ameongeza kuwa: Sisi tumezoea kushuhudia mambo hayo na hatuuoni uadhama na umuhimu wake machoni mwetu, lakini uhakika huo wenye mvuto unawafanya watu walioko nje na wa nchi nyinginezo kujiuliza maswali mengi na kustaajabishwa sana na mambo hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, matukio na uhakika huu wote wa kuvutia umetokana na fikra za kipekee za mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani Imam Khomeini (quddisa sirruh) na ameendelea na hotuba yake kwa kutoa taswira fupi lakini iliyobeba vitu vingi ya chuo na aidiliojia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh)...

1414335

captcha