IQNA

Rais Rouhani asisitiza kutobadilika misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu

21:50 - February 11, 2015
Habari ID: 2840031
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema malengo na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu haiwezi kubadilika.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo hapa Tehran alipohutubia halaiki kubwa ya wananchi katika sherehe za kuadhimisha mwaka wa 36 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, taifa la Iran kama ambavyo lilisimama kidete na kutetea uhuru katika vita vya  kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, mara hii pia linatetea haki zake mbele ya madola makubwa ya dunia katika meza ya mazungumzo ya nyuklia. Rais Rouhani ameongeza kuwa, serikali yake itatekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi katika sekta za uchumi, utamaduni na jamii. Akiashiria mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa  duniani, Rais Rouhani amesema madola ya Magharibi yanadai kuwa vikwazo vimeifanya Iran isalimu amri na kuongeza kuwa iwapo madai hayo ni ya kweli basi kwa nini madola hayo hayaendelezi vikwazo na ni kwa nini yamekuja katika meza ya mazungumzo kwa lengo la kujadili kuondolewa vikwazo hivyo?
Akizihutubu nchi za Magharibi Rais Rouhani amezitaka zikiri kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa kuamiliana vizuri na taifa adhimu la Iran. Rais wa Iran ametangaza bayana kuwa utulivu na amani itapatikana Mashariki ya Kati kwa kushirikishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Rouhani amesema mazungumzo ya nyuklia ni kwa maslahi ya dunia nzima.
Rais Rouhani ameongeza kuwa, kwa bahati nzuri wananchi wa Iran wameshiriki kwa wingi zaidi katika maadhimisho ya tarehe 22 Bahman mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wananchi wa Iran wanaheshimu malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu una Imam Khomeini (MA) na wana azma ya kweli ili kuvuka matatizo yote yanayowakabili. Rais Rouhani ameeleza kuwa kwa kuwepo umoja na mshikamano, Iran inaweza kufikia ustawi na pia kuzisaidia nchi majirani zake. Kwingineko katika hotuba yake Rais Rouhani amesema kufuatia juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumeanza kushuhudiwa kupungua chuki dhidi ya Uislamu duniani. Amesema barua ya hivi karibuni ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa vijana wa Ulaya na Amerika ya Kaskazini ni ishara kuwa Iran inafuata mantiki ile ile ya Imam Khomeini MA.../mh

2834856

captcha