IQNA

Mapinduzi ya Kijeshi Uturuki, Fethullah Gulen, Uislamu wa Kimarekani

12:11 - July 17, 2016
Habari ID: 3470457
Ijumaa usiku Uturuki ilikuwa medani ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli kuiangusha serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Reccep Tayyib Erdogan.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, kufuatia mapinduzi hayo yaliyofeli, vyombo vingi vya habari nchini humo vilimtaja Fethullah Gulen kuwa kinara wa mapinduzi hayo ambayo yalipekekea watu zaidi ya 365 kuuawa, wengi wakiwa wanajeshi waasi, na wengine zaidi ya 1440 kujeruhiwa.

Serikali ya Uturuki imemnyoshea kidole cha lawama Gullen ambaye ametajwa kuwa kiongozi wa serikali kivuli ya Uturuki na mwenye ushawishi mkubwa katika vyombo vya usalama, jeshi na vyombo vya mahakama. Hata baadhi ya wanachama wa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi wanaripotiwa kuwa chini ya ushawishi wake.

Fethullah Gulen anajitambulisha kama msomi wa Kiislamu ambaye anadai kuwa mwenye kufuata 'Uislamu wa Wastani.' Gulen anafuata Uislamu ambao unategemea fikra za Kimagharibi na ambao unahimizwa na Marekani.

Hivi sasa Gulen anaishi uhamishoni nchini Marekani na anapanga kuzindua kitabu kuhusu kile anachokitaja kuwa ni 'Uislamu wa Misimamo ya Wastani'. Gulen anadai kuwa fikra zake zinatokana na mafunzo ya Said Nursi aliyeaga dunia mwaka 1960. Weledi wa mambo wanasema Gulen anatumia jina la mwanazuoni huyo kwa maslahi yake binafsi. Sheikh Nursi aliyezaliwa mwaka 1878 na ambaye sasa ni mashuhuri kwa lakabu ya Badī' al-Zamān Nursi ni kati ya wasomi waliokuwa na taathira katika mwanzo wa kuanza duru za mfumo wa jamhuri muongo wa 20. Harakati na hotuba zake zilipelekea serikali ya kisekula ya Kamal Ataturk kumbaidisha. Ameandika tafsiri maarufu ya Qur'ani ijulikanayo kama Risale-i Nur ya Jildi 13.

Hivi sasa Gulen ana shule 300 nchini Uturuki na kote duniani ameanzisha shule zaidi ya 1000 ambazo pia ziko Afrika Mashariki. Nchini Kenya shule hizo zinajulikana kama Turkish Light na Tanzania ni maarufu kama Feza. Shule zote zilizoanzishwa na Gulen duniani zinatoa mafunzo kwa lugha ya Kiingereza na pia wanafunzi pia husoma lugha ya Kituruki. Rais Erdogan sasa anajaribu kuchukua udhibiti wa  shule hizo duniani na moja ya malengo ya safari yake hivi karibuni barani Afrika ilitajwa ni kuhakikisha kuwa shule hizo zinaendeshwa kwa matakwa ya serikali ya Ankara au zinafungwa.

Kufuatia kufeli mapinduzi ya kijeshi Uturuki, Gulen amekanusha madai ya viongozi wa Ankara na kusema hajahusika na mapinduzi hayo. Lakini iwapo itabainika kweli kuwa alihusika na mapinduzi Uturuki basi ni wazi kuwa ana ushawishi mkubwa katika mfumo wa utawala nchini humo zaidi ya ilivyokuwa kidhaniwa.

Uislamu unahohimizwa na Gulen ni mfano wa wazi wa Uislamu wa Kimarekani. Uungaji mkono wa Marekani kwa Fethullah Gulen bila shaka ni kwa madhara ya Uislamu.

Iwapo mtu kama Gulen atachukua usimamizi wa taifa, ni nini kitajiri? Waislamu wataongozwa kuelekea kutii matakwa ya madola ya Magharibi na watakuwa 'Waislamu wazuri' kwa mtazamo wa Kimagharibi. Kwa maneno mengine watakuwa si tishio lolote kwa madola ya kibeberu na kiistikbari duniani na hata wataruhusiwa kuanzisha 'utawala wa Kiislamu' lakini kwa msingi isiyokuwa ya Kiislamu! Hili ni jambo ambalo nchi za Magharibi zimekuwa zikifuatilia kwa muda mrefu.

Matukio ya hivi karibuni Uturuki yatakuwa na taathira kubwa katika mustakabali wa nchi hiyo. Kuruhusiwa magaidi kupita nchini humo bila kuchukuliwa hatua, na kwa upande mwingine hujuma za kigaidi katika miji mbali mbali ya Uturuki ni mambo yanayotia wasi wasi mkubwa.

Hivi sasa Uturuki inapitia katika kipindi kigumu sana. Nchi hiyo inakabiliana na upanga wenye ncha mbili, kwanza ni kuibuka watu wenye misimamo ya kufurutu ada na isiyo sahihi kwa mtazamo wa mafundisho ya Kiislamu na katika upande wa pili ni kuwepo waungaji mkono wa Uislamu wa Kimarekani unaohimizwa na Gulen. Nukta hizo mbili zimepelekea Uturuki kukabiliana na hali ngumu na mustakabali uliojaa utata.

3515390

captcha