IQNA

Kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni ni sawa na kuisaliti Qur'ani Tukufu

20:05 - August 17, 2020
Habari ID: 3473078
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu amesema kuwa: kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuisaliti Qurani Tukufu na kumpa mgongo Mtume wa Mwenyezi, Muhammad SAW

Hujjatul Islam wal Muslimin Dkt. Hamid Shahriari ameashiria mapatano yaliyofikiwa kati ya Umoja wa Falem za Kiarabu (UAE) na Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili na kusema kuwa: "Baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wanapuuza masuala ya kiitikadi, kibinadamu na kisiasa na wameamua kutangaza waziwazi suala la kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel unaouwa watoto wadgo."

Dkt. Hamid Shahriari amelaani hatua ya UAE ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni na kueleza kuwa, utawala ghasibu wa Isrel unatumia uwezo wake wote wa kijeshi, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi kukabiliana na Ulimwengu wa Kiislamu, kufanya mauaji na ukandamizaji.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu amelitaja suala la kudhalilika Waarabu kuwa ni matokeo ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa: Jambo baya zaidi linaloweza kufanywa na Muislamu katika maisha ni kupoteza Akhera yake ili mtu mwingine afaidike na dunia; na hii ni ishara ya udhaifu wa nafsi katika baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu.  

Alhamisi iliyopita Abu Dhabi na Tel Aviv zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia kufuatia jitihada za Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kufanikisha mwenendo wa kuanzisha uhusiano kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni. 

Mapatano hayo ya UAE na Israel yamepingwa na kulaaniwa vikali na makundi ya mapambano ya Palestina, nchi za eneo la magharibi mwa Asia na shakhsia mbalimbali wa kisiasa duniani. Wapigania uhuru hao wameyataja mapatano hayo kuwa ni usaliti kwa malengo ya Palestina. 

3916947/

captcha