IQNA

Ibada ya Hija

Mahujaji Wairani washiriki katika mjumuiko wa kujibari na washirikina

16:37 - July 09, 2022
Habari ID: 3475482
TEHRAN (IQNA)- Mahujaji Wairani wameshiriki katika mjumuiko wa kujibari na kujiweka mbali na washirikina (bar’aat min-al-mushrikeen) siku ya Ijumaa wakati wa Ibada ya Hija mwaka huu wa 1443 Hijria Qamaria

Ummati mkubwa wa Mahujaji wa Kiirani sambamba na kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina, lakini umekosoa pia njama ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sehemu ya taarifa iliyosomwa na Mahujaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakiwa katika viwanja vya Arafa jana Ijumaa inasema: Ukombozi wa Quds Tukufu kilipo Kibla cha kwanza cha Waislamu, kutoka kwenye mikono ya utawala unaotenda jinai wa Kizayuni na unaoua watoto, ni jambo la dharura na kipaumbele kwa umma wa Kiislamu.

Wametangaza uungaji mkono wao kwa taifa la kimuqawama la Palestina, sanjari na kulaani mpango wowote wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Hapo jana, Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia walisimama katika uwanja wa Arafa, kisimamo hicho kikiashiria kilele cha ibada tukufu ya Hijja. 

Amali ya kujibari na kujiweka mbali na mushirikina ambayo maana yake ni kuchukizwa na kila aina ya uonevu, udhalimu, ubaya, ufisadi wa mataghuti wa zama zote, na kusimama kidete mbele ya wanaotumia mabavu, na mustakbirina  wa zama hizi, ni moja kati ya baraka za Hija na fursa kwa Waislamu ambao mataifa yao yanadhulumiwa.

Katika sehemu nyingine ya taarifa yao, Mahujaji wa Iran wamezikosoa Marekani na utawala wa Kizayuni kwa kula njama za kupanda mbegu za chuki miongoni mwa Waislamu.

Kadhalika Mahujaji hao wa Jamhuri ya Kiislamu wameutaka umma wa Kiislamu kufungamana na mafundisho ya Qurani Tukufu na Mtume Muhammad SAW.

Leo kujiweka mbali na mrengo wa shirki na kufri, ambao ni mrengo wa mustakbirina, kinara wake akiwa ni Marekani, kuna maana ya kujiweka mbali na mauaji yanayotekelezwa dhidi ya wanaodhulumiwa na pia kuna maana ya kujiweka mbali na uenezaji vita; kuna maana ya kulaani vitovu vya ugaidi kama ule ugaidi  wa Daesh (ISIS) na Blackwater ya Marekani; kuna maana ya umma wa Kiislamu kueneza hofu na wahka katika utawala wa Kizayuni na waitifaki wake, huu ni utawala wenye kuua watoto; kuna maana ya kulaani sera za kupenda vita za Marekani na waitifaki wake katika eneo nyeti la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini ambalo mataifa yake yamekumbwa na masaibu na matatizo na kila siku yanakabiliwa na maafa makubwa; kuna maana ya kuchukizwa na ubaguzi kwa msingi wa jiografia, kaumu au rangi ya ngozi; kuna maana ya kuchukizwa na tabia za kiistikbari na khabithi za  madola makubwa vamizi na fitina zinazotekelezwa dhidi ya wale wenye uungwana na uadilifu ambao Uislamu unataka wote wafuate.

 
 
captcha