IQNA

Siasa

Tunisia yatakiwa kuheshimu Sharia ya Kiislamu kwa kuwaachilia wafungwa wa kisiasa

18:40 - June 09, 2023
Habari ID: 3477123
Kampeni imeanzishwa na wasomi wa Kiislamu wanaotaka kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa nchini Tunisia. Miongoni mwa wafungwa wa kisiasa ni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Ennahda, Rashid Ghannouchi.

Takriban wanafikra 150 wa Kiislamu wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS), Sheikh Ali Al-Qaradaghi, wameitaka serikali ya Tunisia kuwaachilia mara moja wafungwa hao, kurejesha uhuru wao, kulinda utu wao na kuheshimu haki zao.
Katika taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, walisema: "Sisi, wasomi na wanafikra wa Ummah, tunaeleza mshikamano wetu kabisa na Profesa Rashid Ghannouchi, mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu na Spika wa Bunge aliyevunjwa, pamoja na wafungwa wote wa kisiasa. Tunataka waachiliwe huru mara moja, kurejeshwa kwa uhuru wao, kuhifadhiwa kwa utu wao, na kuheshimiwa haki zao." Wanazuoni hao wamesisitiza kuwa wito wao ni kwa muhibu wa Sharia za Kiislamu na maadili jumla ya ubinadamu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Tunathibitisha msimamo wetu thabiti katika kuunga mkono haki za binadamu na uhuru wa kimsingi, ambao tunauzingatia kuwa miongoni mwa malengo ya Sharia  za Kiislamu. Katika muktadha huu, tunasisitiza umuhimu wa hatua za pamoja na ushirikiano ili kufikia malengo haya adhimu, ambayo kimsingi ni kulinda uhuru na heshima ya binadamu."
Wanasiasa wengi na wanaharakati wa haki za binadamu duniani kote wametoa wito wa kuachiliwa kwa Ghannouchi. Mwezi uliopita, wasomi 150, wakiwemo Noam Chomsky, Francis Fukuyama na Burhan Ghalioun, walituma barua ya wazi kwa mamlaka ya Tunisia kuwataka kurejesha demokrasia na kuwaachilia wafungwa wa kisiasa.

Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, askari usalama wa Tunisia walivamia nyumba ya kiongozi wa chama cha Ennahda, Ghannouchi, na kumpeleka gerezani. Tangu wakati huo, ofisi zote za chama hicho zimefungwa nchini Tunisia.

Itakumbukwa kwamba, kuanzia Julai 2021, Rais wa Jamhuri ya Tunisia, Kais Saied, alipiga marufuku shughuli za vyama vya siasa na kufanya mabadiliko katika katiba, suala lililochochea mzozo wa kisiasa nchini humo. Kais Saied pia amelivunja Bunge la Taifa la kutwaa madaraka yote ya nchi, jambo ambalo limepingwa na vyama vya siasa vinavyosema hatua za kiongozi huyo ni mapinduzi dhidi ya katiba na demokrasia changa ya nchi hiyo.

3483865

 

captcha